Historia

Ijue Parokia

Historia ya Parokia

HISTORIA YA KANISA KATOLIKI NTYUKA MWAKA 1957 – 2021.

Kanisa katoliki Ntyuka lilianzishwa mwaka 1957 chini ya usimamizi wa kiongozi wa kwanza Mwalimu Jeremiah Raiboni Chomola likiwa na waumini watatu waliokuwa wakisali chini ya mti aina ya mgunga na waumini hao kwa majina waliitwa;

  1. Antoni Yona.
  2. Margareth Nhoi.
  3. Nduche Sila.

Wakristo hawa wakiongozwa na Roho mtakatifu walifanikiwa kujenga kikanisa kidogo cha tembe ikiwa ni nyumba ya asili iliyotumika kwa ibada na sala. Pia ilisaidia kujikinga kwa jua, upepo na mvua wakati wa masika ukilinganisha na sehemu ya awali waliyokuwa wakisali chini ya mti. Wakati huo makao makuu ya kanisa katoliki Dodoma yakiwa Bihawana ambapo Askofu Antoni Jeremiah Penze alipokuwa akikaa na Ntyuka ilikuwa ikihudumiwa na Padre Nobeto, Reginod na Kandido wakitokea Bihawana kwani eneo lote liliitwa parokia ya Dodoma kwa wakati huo. Wamisionari wakifanya kazi ya uinjilishaji/uenezaji injili Afrika wakisaidiana na mapadre wazalendo Stivini Mlundi na Sevelini Supa na Jemes Milto.

Kutokana na ongezeko la wakristu mwaka 1960, iliamuliwa kujenga kanisa na ujenzi huu ulianza chini ya padre Viligidyo mpaka kukamilika kama picha ya muonekano wa kanisa la kwanza ikiwa nyumba ya ibada iliyotumika kufanyia ibada na sala.

Baada ya kukamilika ujenzi wa kanisa hili uliundwa uongozi wa kwanza kusimamia shughuli za maendeleo ya kanisa kwa majina ifuatavyo:-

  1. Antoni Yona.
  2. Margather Nhoyi.
  3. Justini Mesai.
  4. Mjelwa Nhoi.
  5. Anjelina Shaulu.
  6. Lucas Masukuzi.
  7. Legina Chisumbili.

Chini ya uongozi huu ukishirikiana na mwalimu Jeremiah Raiboni Chomola na mapadre wamisionari kutoka makao makuu ya jimbo Bihawana waliokuwa wanakuja kutoa huduma hiyo ya kiroho hapa Ntyuka.

Pamoja na kufanya kazi za kiroho viongozi hawa walikaa na kupanga mipango ya kupata cha fedha kwa ajili ya kuimalisha kazi za kanisa.

Ulianzishwa mradi wa kwanza ambao ilikuwa waumini wa kanisa hili walikuwa wakilima mashamba ya watu na kupata malipo ya fedha zilizotumika kusaidia huduma ya kanisa kwa kipindi hicho waliendelea kufanya kazi za kanisa kwa ushirikiano mkubwa mwaka 1970. Mwalimu Jeremiah Raiboni Chomola alipatikana na hatia ya kosa la kumpiga mwizi wa mifugo yake iliyopelekea kupata adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Hali hii ilileta simanzi kwa waumini kwani mwalimu huyu alikuwa kiungo katika kusalisha na kuwaongozawaumini. Hata hivyo Roho wa bwana alimwinua muumini mmoja aliyeitwa kwa jina Aniselumu akaanza kuliongoza kanisa hili kwa nafasi ya mwalimu wa kanisa kusainiwa na ndugu Antoni Yona.

Mwaka 1971 Mwalimu Jeremiah Chomola alimaliza adhabu ya kifungo na kurejea nyumbani. Na akaendelea kufanya kazi ya kanisa kwa nafasi yake kama mwalimu na jina mwalimu wa kanisa ndilo lilikuwa likifahamika na kutumika kwa wakati huo badala ya katekista.

Mwaka 1972 kanisa la jimbo lilipata msiba mkubwa wa kufariki kwa Baba Askofu Antonio Jeremiah Pence aliyekuwa Askofu na misionari wa kwanza kuliongoza jimbo la Dodoma. Mwaka 1972 alichaguliwa na kuwekwa wakfu askofu Mathias Isuja Joseph kuwa mwananchi na mzalendo wa kwanza kuliongoza jimbo la Dodoma.

Hivyo kanisa lilianza kupata huduma za kiroho chini ya usimamizi wa mapadre wazalendo. Kutokana na ongezeko la waumini mwaka 1976 ilianzishwa kwaya ya kwanza ikiwa na idadi ya wanakwaya 60  ikifundishwa na ndugu Pascal Chilasi kwa merodi ya kienyeji. Kwaya hii ilihamasisha vigango mbalimbali vya parokia ya mt. Paul wa msalaba kama ifuatavyo:-

Mhande, Mkonze, miganga, mzuguni mpinga lugala, mpunguzi ihumwa, misis, msalato, veyulana michese. Vigango hivi ndivyo vilivyokuwa vinaunda parokia yetu ya mt. Paul wa msalaba kwani hapakuwa na parokia yeyote Zaidi ya parokia ya kanisa kuu ndani ya maeneo haya.

Hivyo kanisa hili la Ntyuka limeamsha Imani katika maeneo haya na kupelekea kusimikwa kwa parokia zote zinazoizunguka parokia ya kanisa kuu. Mwaka 1984 baba paroko Ignas Iduri alimteua ndugu Stephen Mombo kuwa msaidizi wa katekista Jeremiah Chomola ambapo walifanya kazi pamoja za kuendesha ibada mafundisho ya dini katika shule ya msingi Ntyuka na kufundisha masakramenti mbalimbali ya kanisa.

Baba paroko Ignas Iduri kama anavyoonekana katika picha alisimamia na kushauri maendeleo ya kanisa hili na kuweka msukumo mkubwa wa kuchagua baraza la kusimamia shughuli za kanisa kama ifuatavyo

  1. Joseph Mombo M/kiti
  2. Salome Mjelwa Mkamu
  3. Edwaed Lamali Katibu
  4. Julius Chinyoyo Makamu katibu.
  5. Sophia Mazengo mweka hazina.
  6. Catherine Chomola Makamu.

Wajumbe:-

  1. Ameria Paul-mjumbe
  2. Antoni Yona-Mjumbe.

Baraza hili liliendelea kufanya kazi za kanisa chini ya mlezi baba paroko Ignas Iduri na tarehe 5.2.1986 iliandikwa barua kumbukumbu No. Kg/NTY/PR/KK/126 kwa uongozi wa serikali ya kijiji cha Ntyuka kuomba kupimiwa eneo la kanisa.

Uongozi wa serikali ya kijiji uliridhia ombi hilo na kutuma ujumbe kwa barua kumb. No. CCM/T/NTY/DM/9/3 ya tarehe 27.2.1986 ukiongozwa na ndugu Daniel Mlindo mjumbe wa halmashauri kuu ya tawi na ndugu Eliza Lubeleje mkuu wa mtaa. Kwa ushirikiano na viongozi wa kanisa hili walipima eneo kwa mapana na marefu kufuatia sheria ya hati miliki ya vijiji vya ujamaa ya mwaka 1972. Walioshiriki upimaji wa eneo la kanisani.

  1. Daniel Mlindo – mjumbe wa halmashauri ya ccm tawi.
  2. Eliza Lubeleje – mkuu wa mtaa.
  3. Jeremiah Chomola – katekista.
  4. Staphani Mombo – katekista msaidizi.
  5. Joseph Mombo – Mwenyekiti.

Na wote waliokuwa wanaishi karibu na eneo la kanisa walikaribishwa kushuhudia upimaji huo ukifanyika.

Baba paroko Ignas Iduri kwa niaba ya waumini wote wa kigango cha Ntyuka aliishukuru halmashauri ya serikali kupitia ofisi ya tawi la CCM Ntyuka kulipatia kanisa eneo la kutosha ambalo litatumika kwa maendeleo ya kanisa. Mwaka 1984 Baba paroko Ignas Iduri alishauri kuwa kigango hiki kinatakiwa kuwa na msimamizi. Akapendekeza msimamizi wa kwanza wa kigango hiki awe MT. GEMMA GALGANI ambaye aliendelea kuwa msimamizi. Kama picha yake inavyoonekana hapa.

Tarehe 12.3.1984 kupitia kikao cha halmashauri ya Baraza waliona idadi ya waumini imeongezeka na kufikia 132 hivyo kanisa lililopo halitoshi na waumini wangine kusalia nje. Iliamuliwa kwa kikao hicho kujengwa kanisa la kudumu baada ya tangazo hili kutolewa kanisani liliungwa mkono na waumini na kupata Baraka ya Baba paroko Ignas Iduri.

Kazi ya ujenzi wa kanisa hili iliendelea kwa michango kutoka kwa waumini wenyewe na kujitolea kufanya kazi na kulima mashamba ya waumini ili kupata fedha za kununulia vifaa vya ujenzi. Mzee Habel Mjelwa Nhoi ni mmoja wa wadau aliyesaidia kutoa kazi za kulima mashamba yake na kulipatia kanisa mifugo iliyouzwa na kupata fedha za kununulia saruji hivyo ametoa mchango mkubwa sana katika kanisa hili. Tarehe 24.5.1987 lilichaguliwa baraza la walei la kigango cha Ntyuka likiwa na muundo ifuatavyo:-

  1. Julius Chinyoyo – M/kiti
  2. Gaitani Mnyapala – Makamu/ m/kiti.
  3. Salome Mjelwa – Katibu.
  4. Paul Mahenge – Makamu Katibu.
  5. Elfrida Mwinyikando – Makamu katibu.
  6. Leah Mnyanzaga – Mweka Hazina.
  7. Milika Mombo – Mweka hazina msaidizi

WAJUMBE.

  1. Lucas Masukuzi
  2. Pascal Chilasi
  3. Hatharina Chomola
  4. Hatharina Lewanga.
  5. Jemma Jumbe.

Baraza hili liliendelea kufanya kazi za kanisa chini ya ulezi na mshauri wa Baba paroko Ignas Iduri aliyedumu akiwa paroko wa kanisa kuu iliyokuwa na vigango 12 avihudumia kama ifuatavyo:-

  1. Ntyuka, 2. Miganga, 3.Mkonze, 4. Zuzu, 5. Madeli, 6. Michese, 7.Segu, 8. Lugala, 9. Nhonhona, 10. Mpunguzi, 11. Nzuguni, 12. Ihumwa.

Wakati huo huduma ya misa takatifu ilikuwa ikitolewa mara moja kwa mwezi kwa kila kigango kwa mzunguko wa vigango vyote ilifanya kigango kimoja kupata misa moja kwa mwaka mzima.

Katika kuendeleza ujenzi wa kanisa hili kwa misingi ya Imani na kuombea miito mbalimbali ya kanisa. Kigango cha ntyuka kimefanikiwa kutoa watawa wawili ambao ni Sr. Michael Mombo na Sr. Kisavera Yona ambao wawili hawa hutoa huduma ya utume wao katika parokia ya chikukwe iliyopo jimbo la Tunduru masasi kama wanavyoonekana katika picha.  Hata hivyo kigango hiki kimetoa wito kwa vijana Damiani Mtanduzi ambaye hayupo katika picha hii anayesoma mwaka wa kichungaji seminari ya Segerea.

Ujenzi wa kanisa hili ulianza 1984, kama historia ilivyoonyesha kwa kutumia nguvu kazi na michango ya waumini wenyewe wa kigango hiki, kutokana na nguvu ya michango ya ujenzi wa kanisa kwenda taratibu kulingana na uwezo wa waumini. Baraza lilitafuta mbinu mbalimbali za kupata fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kufanya harambee ndogo ndogo za kuwaalika wadau kutoka nje na ndani tukishirikiana na uongozi wa parokia yetu ya mt. Paul wa msalaba.

Tarehe 03.02.2002 ilifanyika ibada ya kumuombea Hayati Julius .K. Nyerere Baba wa Taifa, Familia hii iliwakilishwa na marehemu Rosemary Nyerere na mgeni Rasmi alikuwa Anna Abdallah waziri wa Afya akimwakilisha spika wa Bunge Mheshimiwa Pius Msekwa aliyealikwa kuwa mgeni rasmi na ibada ya misa Takatifu iliongozwa na makamu wa Askofu padre Michael Gaula. Baada ya misa ilifanyika harambee kuchangia ujenzi wa kanisa hili ikiwa ni juhudi na lengo kukamilisha ujenzi huu.

Hivyo mpaka kufikia hatua ya kukamilisha ujenzi wa kanisa hili kwa hatua ya awali na kuanza kutumika. Thamani ya fedha zilizotumika ni Tsh. 7,324,544.00 ikiwemo nguvu kazi ya waumini wenyewe.

Mwaka 2017 Mhashamu Askofu Mathiasi Isuja Joseph mstaafu kwa ruksa ya Baba Askofu Yuda Thadei Ruaichi wa jimbo la Dodoma alimpa kibali kukilea na kukisimamia kigango cha Ntyuka chini ya msimamizi wa kigango Mt. Gemma Gargani wakari huo akishirikiana na waumini wa kigango hiki,Akiwa mlezi na msimamizi kwanza alishauri kuwa msimamizi wa kigango Mt. Gemma Gargani ni msimamizi wa jimbo letu la Dodoma. Hivyo ninawaomba tubadilishe msimamizi wetu kwa makubaliano na waumini chini ya ushauri wake Baba yetu wa kiroho alituchagulia msimamizi wa kigango kuwa Mwenyekheri Vichenza Maria Paloni. Waumini wote tulimpokea na kukubali awe msimamizi wetu mpaka leo.

Kanisa hili likiwa na hadhi ya kigango liliendelea kuwa chini ya usimamizi wake mhashamu Askofu Mathias Isuja Joseph (marehemu), mpaka ikawa parokia teule kwa tamko la Askofu wa jimbo la Dodoma Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaia.

Kanisa katoliki teule la ntyuka linaendelea kukua kiimani na mijitoleo mbalimbali chini ya viongozi wa kiroho waliotoa utume wao kwaajili ya ustawi wa kinisa hili na kulifikisha kuwa parokia rasmi leo tarehe 12/12/2021 likiwa chini ya usimamizi wa shirika wa mama Maria wa kana.